Jaribio
jingine la maombi ya dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema),
Godbless Lema linafanyika leo baada ya kusota mahabusu tangu akamatwe
mkoani Dodoma Novemba 3.
Lema
anayekabiliwa na tuhuma ya kutoa lugha ya uchochezi dhidi ya Rais John
Magufuli, ombi hilo la dhamana linakuwa la tatu baada ya kukwama mara
mbili tangu alipoingizwa mahabusu.
Lema
ambaye anatetewa na mawakili sita; Peter Kibatala, John Mallya, Charles
Adiel, Adam Jabir, Faraja Mangula na Sheck Mfinanga, dhamana yake licha
ya kutolewa na Hakimu Mkazi, Desdery Kamugisha ilipingwa kutokana na
notisi ya rufani iliyowasilishwa na mawakili wa Serikali.
Baada
ya notisi hiyo, Lema aliandika barua Mahakama Kuu kuomba mapitio ya
kesi hiyo kwa maelezo kuwa taratibu za kisheria zilikiukwa kutokana na
hakimu kutoa dhamana lakini akashindwa kukamilisha masharti ya dhamana
na kupokea hoja za Jamhuri.
Hata
hivyo, wakili mwandamizi wa Serikali, Paul Kadushi aliwasilisha
pingamizi jingine kupinga Mahakama Kuu kufanya marejeo ya kesi hiyo.
Kadushi
aliwasilisha hoja mbili za kisheria juu ya kuweka pingamizi la ombi la
mbunge huyo kuwa muombaji hakukidhi vigezo vya kuiomba mahakama irejee
maamuzi ya mahakama kwa kuwa badala ya kuiandikia mahakama barua ya
kuomba ifanye mapitio ya maamuzi hayo, angetakiwa akate rufaa juu ya
maamuzi ya mahakama.
Pia,
alisema maombi hayo yamekinzana na Sheria ya Mahakama za Hakimu kifungu
(43) (2) kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kupokea ombi
ama kukata rufaa kwa maamuzi hayo, kwa kuwa ni madogo.
Hata
hivyo, mawakili wa Lema walipinga hoja hizo na kueleza sheria
zinaruhusu mlalamikaji kuandika barua kuomba mapitio, na tayari suala
hilo limewahi kufanyika hata kwa ofisi na mwanasheria mkuu kuomba
mapitio.
Wakili
Kibatala alisema Mahakama Kuu ina mamlaka ya kisheria yenyewe kufanya
mapitio ya kesi hata kama hakuna aliyelalamika na tayari imewahi kufanya
mapitio kwa kesi kadhaa.
Baada
ya hoja za pande zote kutolewa Jaji Sekela Moshi aliomba kupewa muda,
kupitia hoja zote zilizoletwa na pande zote ili kuzifanyia maamuzi leo.
No comments:
Post a Comment