Tuesday, 8 November 2016

Chadema watinga Mahakama Kuu kutaka Lema ashtakiwe














































Mwanasheria wa chama hicho, John Mallya jana aliwaambia waandishi wa habari katika viwanja vya mahakama hiyo kuwa wamefungua kesi hiyo kwakuwa sheria inaelekeza mtuhumiwa kutozidi saa 24 mahabusu bila kufikishwa mahakamani, hivyo kitendo cha kumshikilia Lema kwa zaidi ya muda huo ni kinyume cha sheria.

Katika kesi hiyo, chama hicho kimeiomba Mahakama kuwaamuru Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkuu wa Polisi wa Arusha na Mkuu wa kituo cha Arusha (Central) kumpeleka mahakamani mbunge huyo.

Mallya aliongeza kuwa anakamilisha mchakato wa kukusanya hati ya wito wa kuitwa mahakamani kwa vigogo wa Polisi pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili waweze kueleza ni kwanini wamekiuka masharti ya kisheria ya kutomshikilia mtu kwa zaidi ya saa 24 bila kumfikisha mahakamani.

“Tunataka hawa tuliowashtaki kumleta Lema mahakamani na dhamana yake ifanyiwe mchakato Mahakama Kuu na waiambie mahakama kwanini wasichukuliwe hatua za kisheria, pia tumeomba gharama zote za hii kesi zilipwe na Serikali,” Mallya aliwaambia waandishi wa habari.

Lema alikamatwa Jumatano iliyopita akiwa Bungeni mjini Dodoma na kusafirishwa hadi jijini Arusha kwa tuhuma za kutoa maneno ya kichochezi dhidi ya Rais John Magufuli.

No comments:

Post a Comment