Kufuatia
uchumi wa Tanzania kuzidi kukua na kushika nafasi ya kwanza kwa ukuaji
uchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki, pamoja na jitihada zake za
kuifanya nchi kuwa na uchumi wa kati kupitia viwanda.
Imechaguliwa
kuwa mwenyeji wa mkutano wa tatu wa kimataifa wa Chama cha Kampuni
Ndogo na za Kati Ulimwenguni unaotarajiwa kufanyika kuanzia Disemba 5
hadi 7, 2016 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julias Nyerere, jijini
Dar es Salaam.
Mkurugenzi
Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Godfrey Simbeye amesema chama
hicho huchagua nchi yenye uchumi mkubwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo na
kwamba kuchaguliwa kwa Tanzania kuwa mwenyeji wake, kunaashiria kuwa
miongoni mwa nchi inayokuwa kiuchumi kwa kasi barani Afrika.
“Tanzania
sasa inaanza kuonekana kuwa na hadhi, hali hii huenda inachangiwa na
utendaji kazi wa Rais John Magufuli, na itakuwa nchi ya tatu kufanyika
mkutano huo unaokutanisha wadau na wamiliki wa kampuni ndogo na za kati
duniani,” amesema.
Amesema
mkutano huo utasaidia kampuni za ndani kujifunza namna ya kutoka katika
kampuni ndogo kwenda za kati na za kati kuwa kubwa.
Amesema pia TPSF itaitumia fursa hiyo kutangaza kwa wageni fursa za uwekezaji zilizopo nchini.
“Mkutano
huo pia utafungua milango ya biashara sababu tunatarajia wageni zaidi
ya 200 kutoka nje, watahitaji malazi, chakula na hata bidhaa nyingine za
ndani. Pia tutawaomba wahudhurie katika maonyesho ya bidhaa za Tanzania
yatakayoanza Disemba 7 hadi 11, 2016 ili wajionee bidhaa zinazozalishwa
nchini,” amesema.
Simbeye
amesema kuwa, tafiti iliyofanywa na serikali mwaka 2013 na kuchapishwa
mwaka huu inaonyesha kuwa kuna viwanda 49,000 ambapo 20,000 ni viwanda
vikubwa.
“Uchumi
wa Tanzania utajengwa na viwanda hasa vidogo ambavyo vitaongeza idadi
ya kampuni ndogo nchini, nchi inapokuwa na kampuni nyingi fursa za
kiuchumi pia huongezeka sababu zinaajiri watu. Taasisi ya Sekta Binafsi
itaendelea kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zilizomo nchini,” amesema.
No comments:
Post a Comment