Saturday, 5 November 2016

Majibu ya JPM kwa wanahabari kuhusu muswada wa Sheria ya Huduma za Habari 2016


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Magufuli amesema kuwa huu ni wakati mwafaka kwa muswada wa sheria ya huduma za vyombo vya habari kukubaliwa na kuwa sheria kwa vile tasnia ya habari inakumbwa na changamoto nyingi zitakazotatuliwa na sheria hiyo.

Akizungumza na wahariri pamoja na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari jana, Ikulu jijini Dar es Salaam Rais Magufuli alisema kuwa muswada huo ni wa muda mrefu na sasa ni wakati mwafaka kwa vile tansia ya habari inakumbwa na changamoto nyingi zinazoweza kutatuliwa na muswada huo.

“Hii sheria ya huduma za vyombo vya habari imechelewa kwa vile mchakato wake ulianza tangu mwaka 2011 hadi sasa mwaka 2016 wadau walikuwa na muda wa kutosha wa kujiandaa na kutoa maoni yao ambayo yangeweza kuboresha muswada huo” alisema Rais Magufuli

Ameongeza kuwa, Sheria hii italeta mabadiliko katika tasnia ya habari kwa vile kutakuwepo na Bodi ambayo itashughulikia masuala ya taaluma ya habari, pamoja na mambo mengine yaliyoanishwa katika muswada huo ambayo ni maslahi ya waandishi wa habari nchini.

Muswada huu unatazamiwa kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili waweze kufanyakazi kitaalamu kwa kuandika na kutangaza habari zenye ukweli zitakazochangia katika harakati za kuleta maendeleo kwa nia ya kuwasaidia watanzania na serikali kwa ujumla katika kufikia malengo yake.

Muswada wa Sheria ya huduma za habari umesomwa jana Novemba 4, 2016 katika kikao cha tano cha Bunge na mkutano wa 11, ambapo utajadiliwa na kufuata taratibu zingine kabla ya kuwa sheria. 

No comments:

Post a Comment