Saturday, 5 November 2016

Rais Magufuli Awataka Watanzania Kutumia Fursa Zilizopo

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amewataka watanzania kutumia fursa zilizopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kwa ajili ya kuliletea maendeleo ya taifa.

Aliyasema hayo jana Jijini Dar es Saalam wakati wa mkutano wake na Wahariri wa vyombo vya habari nchini katika kuadhimisha mwaka mmoja wa Utawala wake, ambapo alisema kuwa ipo haja ya kuzungumza na kuelimisha watanzania juu ya fursa zilizopo katika taasisi hizo.

“Katika Jumuiya hizo zipo fursa nyingi kwa ajili ya maendeleo ingawa inahitajika elimu ya kutosha kwa watanzania kuona fursa zilizopo ikiwemo ufundishaji wa lugha ya Kiswahili nchi za nje” alisema Rais Magufuli.

Mbali na hayo, akizungumza kuhusu suala la kupambana na Rushwa nchini Rais Magufuli alitoa wito kwa vyombo vinavyohusika na kupambana na rushwa kufichua watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo.

Rais Magufuli alisema kuwa vita ya Rushwa ni ya kila mwananchi, ambapo alitoa wito kwa watanzania wote kwa ujumla kujiepisha na masuala ya rushwa kwani rushwa ni kansa ya maendeleo nchini.

“Taifa litakwama tukiacha suala la rushwa liendelee, tumeumia kweli kweli katika hili hivyo nitoe wito kwa watanzania wote kwa ujumla kujiepusha na masuala haya kwa ajili ya maendeleo ya nchi kwani kesi ya rushwa ni yetu sote” alifafanua Rais Magufuli.

No comments:

Post a Comment