Mamlaka
ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) - imeendelea kuwataka Wakulima kufuatilia
kwa ukaribu Taarifa za hali ya hewa pamoja na kuzingatia maelekezo ya
wataalamu wa kilimo.
Hatua
hiyo inatokana na uwepo wa dalili za upungufu wa mvua katika mwezi
Novemba kwenye maeneo mengi nchini jambo ambalo linaweza kuathiri
uzalishaji katika kilimo.
Hayo yamebainishwa jana Jijini
Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini Dkt.
Agnes Kijazi alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari ambapo alisema
hadi sasa bado kuna viashiria vingi vya upungufu wa mvua ikiwa ni
pamoja na kupungua kwa Joto katika eneo la kati la Bahari ya Pasifiki
kitendo ambacho kinafahamika kama LANINA.
Alibainisha
kuwa hali hiyo inapojitokeza husababisha ukame hivyo kwa wakulima
kuzingatia maelekezo ya wataalam wa kilimo kwa kulima mazao ya muda
mfupi na yanayostahamili ukame.
Dkt. Kijazi aliongeza
kuwa Mamlaka hiyo imekuwa ikifuatilia kwa ukaribu mienendo ya ya
unyevunyevu katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na Joto katika Bahari
ya Hindi ambapo imebainika kuwa hali ya unyevunyevu inaendelea kupungua
katika maeneo mbalimbali nchini huku Joto katika Bahari ya Hindi
ikionekana kuendelea kupungua mambo ambayo ni dalili za upungufu wa mvua
na ukame.
Aidha Dkt. Kijazi alizungumzia tatizo la kutokea kwa mvua za mawe katika baadhi ya maeneo nchini ambapo alibainisha
kuwa tatizo hilo linasababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo
hupelekea kutokea kwa aina ya mawingu inayofahamika kama mawingu ng’amba
hivyo suala hilo halina sababu za kuhusianishwa na Imani za kishirikina
kama ambavyo baadhi ya watu wamekua wakidhania.
No comments:
Post a Comment