Monday, 31 October 2016

Rais Magufuli kufanya ziara ya Kiserikali ya siku mbili nchini Kenya Kuanzia Kesho


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 31 Oktoba, 2016 ataanza ziara ya Kiserikali ya siku mbili nchini Kenya kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta.

Rais Magufuli anatarajiwa kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Jijini Nairobi majira ya saa nne asubuhi na baadaye kupokelewa rasmi na mwenyeji wake Rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi ambako viongozi hao watafanya mazungumzo rasmi.

Pamoja na kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Rais Magufuli atakwenda kutoa heshima katika Kaburi la Rais wa Kwanza wa Kenya Hayati Mzee Jomo Kenyatta na pia anatarajiwa kuhudhuria dhifa ya kitaifa aliyoandaliwa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta Ikulu Jijini Nairobi

Katika ziara hii Rais Magufuli anatarajiwa kutembelea kiwanda cha maziwa cha  Eldoville kilichopo Karen Jijini Nairobi, na pia anatarajiwa kuzindua barabara mchepuko ya Southern By-pass iliyopo Jijini Nairobi.

Barabara hiyo mchepuko ya Southern By-pass ni moja kati ya miradi mikubwa ya barabara nchini Kenya, inaunganisha maeneo mbalimbali ya Jiji la Nairobi kwa barabara za juu na chini na imejengwa kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katika Jiji hilo.

Rais Magufuli anatarajiwa kumaliza ziara yake tarehe 01 Novemba, 2016 na kurejea Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment