Wednesday, 9 November 2016

Rais Magufuli Ampongeza Donald Trump Kwa Kushinda Kiti cha Urais Wa Marekani


Leo November 9, 2016 Marekani imeweka historia nyingine baada Donald Trump wa chama cha Republican kutangazwa mshindi wa kiti cha Urais, na tayari ameanza kupokea pongezi kutoka kwa viongozi wa nchi mbalimbali ikiwemo Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli.

Rais Magufuli ametoa pongezi zake kwa Rais Donald Trump kupitia ukurasa wake Twitter

Rais Barack Obama ampongeza Rais Mteule, Donald Trump na kumualika Ikulu kujadiliana juu ya makabidhiano ya ofisi.

Rais Barack Obama wa Marekani  amempongeza Rais Mteule wa taifa hilo, Donald Trump na kumualika Ikulu kujadiliana juu makabidhiano ya ofisi.

Msajili wa vyama vya siasa Tanzania, avifutia usajili Vyama Vitatu

Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania Jaji Francis Mutungi ametangaza kuvifutia usajili vyama vitatu baada ya kubainika kukiuka sheria ya usajili wa vyama.

Vyama hivyo ni pamoja na CHAUSTA kilichopata usajili wa kudumu tarehe 5 Novemba 2001, The African Progressive Party of Tanzania ( APPT-Maendeleo) kilichopata usajili wa kudumu terehe 4 Machi 2003 na Chama cha Jahazi Asilia kilichopata usajili wa kudumu tarehe 17 Novemba 2004.

Jaji Mutungi amesema kuwa mchakato wa kufuta usajili wa vyama hivyo umetokana na zoezi la uhakiki wa utekelezaji wa masharti ya usajili na matakwa mengine ya sheria ya vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu lililofanyika kuanzia tarehe 26 Juni hadi 26 Julai 2016.

Amesema katika zoezi hilo uhakiki ulibaini kuwa vyama hivyo vimepoteza sifa za usajili wa kudumu kwa kukiuka masharti ya sheria ya vyama vya siasa, na kwamba kila chama kilipewa ya nia ya msajili kufuta usajili wake, lakini vikashindwa kutoa utetezi wa kuridhisha ili visifutiwe usajili.

Kufuatia uamuzi huo, Msajili amewataka waliokuwa wanachama wote wa vyama hivyo kutojiuhusisha na shughuli yoyote kwa majina ya vyama hivyo, na kwamba kufanya hivyo ni kuvunja sheria, huku akiviasa vyama vingine kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria.

TRA Yakusanya Shilingi Trilioni 1.15 Mwezi Oktoba

Na Ally Daud-MAELEZO.
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikia kukusanya shilingi trilioni 1.15 kwa mwezi Oktoba ikiwa ni kukamilisha malengo waliyojiwekea katika ukusanyaji wa mapato.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi Bw. Richard Kayombo wakati wa mkutano  na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu  hali ya makusanyo na zoezi la uhakiki wa namba za utambulisho wa mlipa kodi (TIN)linaloendelea hivi sasa.

“Tumefanikiwa kukusanya shilingi Trilioni 1.15 kwa mwezi Oktoba mwaka huu ikiwa ni kufanikisha malengo ya ukusanyaji kodi nchini ili kukuza uchumi wa nchi pamoja kusaidia Serikali kuendeleza huduma za jamii nchini” alisema Bw. Kayombo.

Aidha Bw. Kayombo amesema kuwa mapato hayo yametokana na mikakati thabiti iliyowekwa na mamlaka hiyo katika ukusanyaji kodi hapa nchini ili kuweza kusaidia ongezeko la pato la Taifa .

Katika hatua nyingine TRA imefanikiwa kushinda kesi 9 kati ya 10 zilizokuwa zikiendelea katika mahakama mbalimbali nchini dhidi ya walipa kodi wake na kufanikiwa kupata kiasi cha takribani Bilioni 16.9 .

“Tumefanikiwa kushinda kesi 9 kati ya 10 ambazo zilifikishwa mahakamani dhidi ya walipa kodi na kupata kiasi cha shilingi bilioni 16.9 hivyo kufanya juhudi zetu za kukusanya mapato mengi zaidi” aliongeza Bw. Kayombo.

Mbali na hayo Bw. Kayombo amesema kuwa zoezi la uhakiki wa namba za utambulisho wa mlipa kodi ambalo limeanza hivi karibuni linaendelea na litafikia tamati Novemba 30 mwaka huu kwa mkoa Dar es salaam hivyo wananchi kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya uhakiki huo.

Aidha Bw. Kayombo ameongeza kuwa  kila mwenye namba ya utambulisho wa mlipa kodi anatakiwa akahakiki kwa ajili ya kupata taarifa sahihi za mlipa kodi ili kuepuka kufutwa kwa  namba yake ya utambulisho baada ya zoezi hilo kumalizika kwa mkoa husika.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatano ya Novemba 9

Serikali: Ukosefu wa ajira kwa vijana umepungua

Serikali ya Tanzania imesema kwamba kulingana na takwimu inaonesha kuwa  ukosefu wa ajira kwa vijana nchini Tanzania umepungua kwa asilimia mbili, kutoka asilimia 13.7 mwaka 2012 mpaka asilimia 11.7 mwaka huu.

Akizungumza jana bungeni, mjini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali na majibu Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu Mhe. Anthony Mavunde,  alisema licha ya kupungua huko kwa ukosefu wa ajira, serikali imeweka mipango ya kuwawezesha vijana kuwa na wigo mpana wa ajira nchini.

Mhe. Mavunde alisema kuwa kwa takwimu hizo Tanzania ni nchi inayoongoza kwa kutoa ajira kwa vijana wengi zaidi kushinda baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Kenya na Uganda.

Ratiba ya Mazishi ya Spika Mstaafu, Samwel John Sitta

Mwili wa aliyekuwa spika wa bunge,  Samuel Sitta unatarajia kuwasili nchini siku ya Alhamis ukitokea nchini Ujerumani ambapo alipokuwa akipatiwa matibabu.

Taarifa hiyo imetolewa na Gerald Mongela ambaye ni msemaji wa familia.  
Amesema mara baada ya mwili huo kuwasili nchini utapelekwa nyumbani kwa marehemu Masaki jijini Dar es Salaam na siku ya Ijumaa shughuli za kuaga zitafanyika katika viwanja vya Karimjee kisha kupelekwa bungeni mjini Dodoma.

“Mwili wa mpendwa wetu mheshimiwa Samuel Sitta utawasili na ndege ya Emirates siku ya Alhamis saa tisa na nusu alasiri na baada ya hapo mwili tutauleta hapa nyumbani kwaajili ya kukaa nao na kupumzika kusubiri ratiba ya Ijumaa,”alisema Mongela.

Mazishi ya Marehemu Samwel John Sitta yatafanyika siku ya Jumamosi Urambo mkoani Tabora.