Saturday, 29 October 2016

Mmiliki wa Shule Iliyofutiwa Matokeo Ya Darasa la 7 Amwaga Machozi Hadharani

Siku moja baada ya matokeo ya darasa la saba kutangazwa, baadhi ya wamiliki wa shule wamelijia juu Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kwa kufuta matokeo ya wanafunzi wao, huku mmoja wao akibubujikwa na machozi akidai wamehujumiwa.

Ikitangaza matokeo hayo juzi, Necta ilisema imefuta matokeo ya wanafunzi 238 kwa sababu ya udanganyifu, ikiwatuhumu wakuu wa shule sita na walimu kuhusika kuiba mitihani, kuwapa majibu watahiniwa au kuwafanyia mtihani.

Necta ilienda mbali zaidi na kudai kuwa kwenye shule moja, walimu walijificha bwenini, chooni na ofisini ambako wanafunzi waliwafuata na kupewa majibu na baadaye kuyasambaza kwa wenzao.

Lakini, walimu hao  wamepinga vikali tuhuma hizo za kushiriki katika udanganyifu, isipokuwa shule moja tu ambayo ilisema mwalimu aliyehusika ameshachukuliwa hatua.

“Sijafurahishwa na kitendo cha Necta kuifutia matokeo shule yetu. Hiyo ni hujumu,” alisema mmiliki wa shule ya msingi Tumaini iliyopo Sengerema mkoani Mwanza, Kandumula Maunde.

Huku akilia, Maunde alisema wakati tukio hilo lilotokea saa 5:00 asubuhi, hakuwepo na hakushirikishwa.

“Niliitwa kesho yake na kupata maelezo kuwa wanafunzi wa shule yako wamekamatwa kwa sababu wameandikiwa majibu ya mtihani kwenye sketi, sikukubaliana nao,” alisema.

Kwa mujibu wa Necta, mmiliki huyo aliiba na kuandaa majibu ambayo watahiniwa wake waliandika kwenye sare za shule na kuyatumia ndani ya chumba cha mtihani.

Necta imewataja waliohusika kuwa ni mmiliki aliyetajwa kwa jina la Jafari Maunde, msimamizi anayeitwa Alex Kasiano Singoye na wanafunzi wote.

Alisema hakukubaliana na kitendo hicho kwa sababu wanafunzi hao walikuwa wameandaliwa vizuri kujibu mitihani yao.

Maunde aliliomba baraza la mitihani kupitia upya uamuzi wake wa kuifutia shule hiyo matokeo kwa kuwa umeathiri maisha ya wanafunzi waliokuwa na ndoto za kuendelea na masomo.

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo waliofutiwa matokeo waliiomba Necta kuangalia upya uamuzi huo. Wanafunzi hao walieleza kuwa msimamizi wa mtihani wa siku hiyo alikuwa akiwasumbua na aliwalazimisha waandike maelezo ya kukiri kuwa walikamatwa na majibu.

“Msimamizi alitulazimisha tuandike kwenye ubao baada ya kumaliza mitihani maelezo yakisema tumekamatwa na majibu ya mtihani yakiwa yameandikwa kwenye sketi tulizokuwa tumevaa,” alisema mmoja wa wanafunzi hao, Kefa Matini.

Kwa upande wa shule ya msingi ya Little Flower iliyopo Serengeti mkoani Mara, walimu walisema uamuzi wa kufutiwa matokeo ni adhabu isiyostahili.

Wanafunzi 37 wa shule hiyo  inayomilikiwa na Kanisa Katoliki, Parokia ya Magumu wamefutiwa matokeo. 

Necta imeeleza kuwa mwalimu mkuu wa Little Flowers aliiba mtihani, kuandaa majibu na kumpa msimamizi mkuu pamoja na wasimamizi wengine ili wawape watahiniwa.

Imesema waliohusika ni mwalimu mkuu anayeitwa Cecilia Nyamoronga, msimamizi mkuu (mwalimu), Haruni Mumwi na msimamizi (mwalimu), Genipha Simon na watahiniwa wote.

Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo, Paskael Chacha alisema uamuzi huo umewaumiza walimu na watoto waliofanya mtihani walioko shuleni na wazazi kwa kuwa hawajapewa sababu za udanganyifu huo na ulimhusisha nani na lini.

“Walimu hawakuwepo shuleni, mkuu wa shule ndiye alikuwa akiruhusiwa kuwepo shuleni kwa muda mfupi. Inanipa shida kujua udanganyifu ulifanyikaje na ulimhusisha nani.

"Hili suala linatupa shida kwa kuwa wasimamizi walioletwa siku ya kwanza si waliofika kusimamia. Sasa taarifa kama hizi zinauma sana,” alisema.

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa taarifa zinazodai kuwa siku ya mtihani mtoto mmoja alikamatwa na karatasi ya majibu na kumtaja mkuu wa shule kuwa ndiye aliyempa, mwalimu huyo alikana na kudai kuwa hana taarifa.

Majibu ya Dr. Msonde
Akizungumzia malalamiko hayo, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema wanaosema wameonewa wanatakiwa kuomba radhi na kukubali adhabu kwa sababu waliokamatwa walikutwa na uthibitisho, akitoa mfano wa Shule ya Msingi Tumaini.

Kwa upande wa Shule ya Msingi Little Flower, Dk Msonde alisema ofisa wa baraza la mitihani alishuhudia mwalimu akipitisha karatasi ya majibu kwa wanafunzi .

“Sasa hapo utasema umeonewa? “Tumezoea kuona (matukio ya udanganyifu) yale ya mwanafunzi mmoja, lakini haya yanatisha. Mwalimu au msimamizi anamsaidia mwanafunzi, hii si sawa,” alisema.

No comments:

Post a Comment