Saturday, 29 October 2016

Taarifa ya Mamlaka ya Dawa na Chakula TFDA kuhusu Dawa bandia zilizokamatwa


Na Ally Daud-Maelezo
MADAWA bandia na yasiyo sahihi kwa matumizi ya binadamu yamekamatwa maeneo ya Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini baada ya kufanyika ukaguzi maalum wa kutafuta dawa bandia katika maeneo hayo iliyofanyika hivi karibuni.
 
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Bw. Hiiti Sillo wakati wa kutoa Matokeo ya ukaguzi maalum wa dawa uliofanyika katika mikoa ya Kanda za Ziwa na Nyanda za Juu Kusini.
 
“Kutokana na ukaguzi maalum tulioufanya katika Kanda za Ziwa pamoja na Nyanda za Juu Kusini wa kutafuta dawa bandia na zisizo sahihi kwa matumizi ya binadamu tumefanikiwa kukamata dawa bandia za aina tano ambazo zipo kwenye makundi mawili ya Dawa za malaria na Viua vijasumu(Antibiotics)” alisema Bw. Sillo.
 
Aidha Bw. Sillo amesema kuwa ukaguzi huo maalum umeweza kusaidia kukamata dawa ya malaria aina ya vidonge vya Quinine ambayo inadaiwa kutengenezwa katika kiwanda cha Elys Chemical  nchini Kenya na nyingine zinatengenezwa hapa nchini katika kiwanda cha Shelys Phamaceuticals Ltd.
 
Mbali na hayo Bw. Sillo amesema kuwa pamoja na kukamata dawa bandia pia zoezi hilo lilifanikiwa kubaini na kukamata dawa zilizoisha muda wa matumizi , zisizosajiliwa na zenye ubora duni zenye thamani ya Tsh. Milioni 17.463.
 
Bw. Sillo ameongeza kuwa Ukaguzi huo ulitokana na kuwa na taarifa za awali ambazo zilionyesha uwepo wa dawa bandia katika maeneo ya Geita na Mara mwezi Agosti na Septemba mwaka huu  na kusistiza kwamba zoezi hilo la ukaguzi linaendelea nchini kote na watakaokutwa na hatia watachukuliwa hatua stahiki.
 
Kwa upande wa Msajili wa  Baraza la famasi Bi. Elizabeth Shekalaghe amesema kuwa wataalamu wa madawa watakaokutwa na hatia ya kusambaza na kuhudumia dawa bandia watafutiwa usajili na kuacha kutoa huduma  kwa mujibu wa sheria ya dawa , chakula na vipodozi.
 
“Wataalamu wa dawa ambao wanasambaza na kuhudumia dawa bandia watafutiwa usajili na kuacha kutoa huduma  kwa mujibu wa sheria ya dawa , chakula na vipodozi pindi watapogundulika” alisema Bi. Shekalaghe.
 
Zoezi hilo la Ukaguzi maalum wa dawa bandia ulianza Oktoba 4 mwaka huu linafanywa kwa ushirikiano wa TFDA, Jeshi la polisi pamoja na Maafisa kutoka Baraza la Famasi litakuwa endelevu ili kuhakikisha dawa bandia zinatoweka nchini.

No comments:

Post a Comment