Monday, 31 October 2016

Rais Magufuli alivyowasili Nairobi nchini Kenya


Leo October 31 2016 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli aliondoka nchini kuelekea Nairobi nchini Kenya kwa ziara ya Kiserikali ya siku mbili nchini humo kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Kenya Uhuru Kenyatta.
Rais  Magufuli  amewasili Nairobi kenya kwa ziara hiyo na amelakiwa na mwenyeji wake Rais uhuru kenyatta.
tza-ke-rais-magufuli-nchini-ke
tza-ke-rais-magufuli-nchini-ke-3jpg

Serikali Yazuia Mpango wa Mchungaji Lwakatare na Mrema Kuwalipia Faini Wafungwa

Serikali imesitisha shughuli iliyokuwa ikiendeshwa na Mchungaji Getrude Lwakatare ya kuwalipia faini wafungwa walioko magerezani hadi hapo utaratibu mwingine utakapotolewa.
Mpango huo unaofanywa na Lwakatare kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Taifa wa Bodi ya Parole, Augustine Mrema tayari umewezesha wafungwa 78 kutoka magerezani baada ya kuwalipia faini inayofikia Sh25 milioni. 
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma, Antonio Kilumbi alisema amepata maelekezo ya kusitishwa kwa mpango huo kutoka ngazi ya juu ya jeshi hilo. 
Alisema wananchi wengine bado wanaweza kuwalipia faini hiyo ndugu zao. Mrema alisema jana kuwa mpango huo ulilenga kupunguza msongamano magerezani na kuipunguzia Serikali gharama za kuwahudumia wafungwa.

Lowassa, Sumaye Wapiga Kambi Dodoma Ili Kuteta na Wabunge wa UKAWA


Mawaziri Wakuu wa zamani ambao ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa na Frederick Sumaye wameweka kambi mjini Dodoma ili kuteta na wabunge wa Ukawa.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema kuwa wanasiasa hao wako mjini humo kwa ajili ya kufanya vikao na wabunge wa Ukawa ili kuweka mkakati na msimamo dhidi ya hoja mbalimbali zinazotarajiwa kuibuliwa katika vikao vya Bunge vinavyoanza kesho.

Moja kati ya hoja zinazotarajiwa kuwekewa msimamo ni pamoja na kuupinga muswada wa huduma za habari unaotarajiwa kujadiliwa na kupitishwa kuwa sheria.

“Tutakuwa na kikao cha kuweka msimamo wetu dhidi ya muswada hatari wa huduma za habari,” Mrema anakaririwa. “Vikao vimeshaanza na vitaendelea kesho (leo),”aliongeza.

Kwa mujibu wa Mrema, mbali na Lowassa, Sumaye na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, vigogo wengine wa Ukawa waliohudhuria vikao hivyo ni pamoja na Profesa Mwesiga Baregu, Profesa Abdallah Safari na Arcado Ntagazwa.

Rais Magufuli afanya uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)


Rais wa Jamhuri ya Muunganowa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 30 Oktoba, 2016 amemteua Jenerali Mstaafu George Marwa Waitara kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).

Taarifa iliyotolewa leo na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi huo umeanza tarehe 29 Oktoba, 2016.

Jenerali Mstaafu George Marwa Waitara ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstaafu.

WAKATI HUO HUO,Rais Dkt. Magufuli amemteua Dkt. Eligy Mussa Shirima kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI)

Uteuzi wa Dkt.Shirima umeanza tarehe 29 Oktoba 2016.

Kabla ya uteuzi huu Dkt. Eligy Mussa Shirima alikuwa Mtafiti Mkuu na Msimamizi wa Utafiti wa Nyama ya Ng'ombe Makao Makuu ya TALIRI. 

Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

Rais Magufuli kufanya ziara ya Kiserikali ya siku mbili nchini Kenya Kuanzia Kesho


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 31 Oktoba, 2016 ataanza ziara ya Kiserikali ya siku mbili nchini Kenya kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta.

Rais Magufuli anatarajiwa kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Jijini Nairobi majira ya saa nne asubuhi na baadaye kupokelewa rasmi na mwenyeji wake Rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi ambako viongozi hao watafanya mazungumzo rasmi.

Pamoja na kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Rais Magufuli atakwenda kutoa heshima katika Kaburi la Rais wa Kwanza wa Kenya Hayati Mzee Jomo Kenyatta na pia anatarajiwa kuhudhuria dhifa ya kitaifa aliyoandaliwa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta Ikulu Jijini Nairobi

Katika ziara hii Rais Magufuli anatarajiwa kutembelea kiwanda cha maziwa cha  Eldoville kilichopo Karen Jijini Nairobi, na pia anatarajiwa kuzindua barabara mchepuko ya Southern By-pass iliyopo Jijini Nairobi.

Barabara hiyo mchepuko ya Southern By-pass ni moja kati ya miradi mikubwa ya barabara nchini Kenya, inaunganisha maeneo mbalimbali ya Jiji la Nairobi kwa barabara za juu na chini na imejengwa kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katika Jiji hilo.

Rais Magufuli anatarajiwa kumaliza ziara yake tarehe 01 Novemba, 2016 na kurejea Jijini Dar es Salaam.

Basi La Abiria Lateketea Kwa Moto Kimara Stop Over Jijini Dar......Mtu mmoja Afariki, 16 Wajeruhiwa

Basi lenye namba za usajili T990 AQF mali ya kampuni ya Safari Njema liililokuwa likitokea Dodoma kuja jijini Dar, jana liliteketea kwa Moto maeneo ya Kimara Stop Over-Suka, mara baada ya kugongana na Lori lililokuwa limebeba shehena ya mifuko ya Cement (namba zake za usajili hazikujulikana mara moja).

Imeelezwa kuwa mali zote zilikuwemo katika basi vimeteketea kabisa kwa moto.
 
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa mtu mmoja amefariki Dunia katika ajali hiyo na wengine 16 wamejeruhiwa na baadae kukimbizwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu. 

HESLB Yafafanua vigezo Utoaji mikopo.........Waliokosa sababu zatajwa, wapewa nafasi ya kukata rufaa

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa ufafanuzi kuhusu vigezo inavyotumia katika kuchambua, kupanga na kutoa mikopo kwa wanafunzi 20,183 (asilimia 74) wa mwaka wa kwanza hadi sasa kati ya 25,717 iliyopanga kuwapa mikopo katika mwaka huu wa masomo, 2016/2017.

Idadi iliyobaki (asilimia 26) ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza itajazwa na waombaji ambao baadhi ya nyaraka walizowasilisha zinaendelea kuchambuliwa ili kuthibitisha uhalisi wake na baadhi zitajazwa na waombaji ambao wanakata rufaa na kuwasilisha nyaraka zinazothibitisha uhitaji wao kwa mujibu wa vigezo vya mwaka huu.

Aidha, katika mwaka huu wa masomo, Serikali imepanga kutumia jumla ya Tshs 483 kutoa mikopo kwa wanafunzi 93,295 wanaoendelea na 25,717 wa mwaka wa kwanza.

Katika mkutano na waandishi wa habari jana (Jumapili, Oktoba 30, 2016), Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru alisema vigezo vikuu vinavyotumika mwongozo uliotangazwa na Bodi hiyo wakati ilipotangaza kuanza kupokea maombi mwezi Juni mwaka huu ambao unataja makundi makuu matatu ya watakaopata mikopo.

Vigezo vilivyotumika kutoa mikopo
Kwa mujibu wa Bw. Badru, kundi la kwanza linajumuisha wanafunzi waombaji wa mikopo wenye uhitaji maalum kama wenye ulemavu uliothibitishwa na Waganga Wakuu wa Wilaya na yatima ambao katika maombi yao waliwasilisha nakala za vyeti vya vifo zilizothibitishwa na makamishna wa viapo.

“Kundi la pili linajumuisha waombaji wa mikopo ambao baada ya uchambuzi wa taarifa zao walizowasilisha na baada ya kulinganisha na gharama za jumla za masomo yao ya sekondari, wamebainika kuwa wana uwezo mdogo wa kugharamia masomo yao ya elimu ya juu na hivyo kuwa na uhitaji zaidi wa mikopo,”
alisema Bw. Badru.

Katika mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Bw. Badru alitaja kundi la tatu na la mwisho kuwa linajumuisha waombaji wa mikopo ambao wenye ufaulu wa juu katika matokeo yao ya kidato cha sita na wamechaguliwa kujiunga na fani za kipaumbele kwa taifa.

Fani hizo ni Sayansi za Tiba, Ualimu wa Sayansi na Hisabati, uhandisi wa Kilimo, Mafuta na Gesi na Sayansi za Ardhi, Usanifu Majengo na Miundombinu.

Makundi ya wanafunzi waliopata mikopo
“Hivyo basi, hadi sasa tumetoa mikopo kwa wanafunzi 20,183 wakiwemo wanafunzi yatima 4,321, wenye ulemavu 118, wanafunzi wenye uhitaji waliosomeshwa na taasisi mbalimbali katika masomo ya sekondari (87), wanafunzi wanaosoma kozi za kipaumbele 6,159 na wanafunzi wanaosoma kozi zisizo za kipaumbele lakini wanaotoka kwenye familia duni 9,498,” alifafanua Bw. Badru. 

Sababu za kukosa mikopo
Katika mkutano huo, kiongozi huyo wa HESLB pia alieleza kwa kina sababu nyingine za waombaji 27,053 ambao hawajapangiwa mikopo.

Ametaja sababu hizo kuwa ni pamoja na baadhi ya waombaji (90) kuwa na umri wa zaidi ya miaka 30, waombaji mikopo waliopata udahili kwa sifa linganishi (equivalent qualifications) na waombaji waliomaliza masomo ya kidato cha sita zaidi ya miaka mitatu iliyopita.

Kundi jingine la waombaji waliokosa mikopo katika awamu ya kwanza ni waombaji waliopata nafasi katika vyuo kwa ufaulu wa mitihani waliyofanya kama watahiniwa binafsi (Private Candidates) na waombaji ambao hawakurekebisha fomu zao za maombi ingawa waliitwa kufanya hivyo.

Nafasi ya rufaa na uhakiki wa wanafunzi wanaoendelea na masomo
Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji huyo pia amewataka waombaji ambao hawajaridhika na upangaji wa mikopo unaotangazwa, kuwasilisha rufaa zao kwa njia ya mtandao utakaofunguliwa kuanzia katikati ya wiki hii.

“Tunafahamu kuwa kuna baadhi ya wanafunzi wamekosa mkopo kwa kutowasilisha baadhi ya nyaraka ingawa tuliwaomba kufanya hivyo, hawa na wengine wenye sababu za msingi, watapata fursa ya kuwasilisha rufaa zao kwa njia ya mtandao na nakala kuzituma kwa utaratibu tutakaoutangaza wiki inayoanza kesho(leo),”
alisema Bw. Badru.

Aidha, katika mkutano huo, Bw. Badru alisema bodi ya Mikopo inatarajia kuanza kazi kuhakiki taarifa za wanafunzi wanaoendelea na masomo ambao wanapata mikopo ya elimu ya juu kwa lengo la kubaini kama ni wana uhitaji wa mikopo hiyo kwa mujibu wa vigezo au hapana.

Katika zoezi hili linalotarajiwa kufanyika kwa siku 30 kuanzia mwezi ujao (Novemba, 2016), wanafunzi wote ambao ni wanufaika watalazimika kujaza dodoso maalum litakalokusanya tarifa za kiuchumi za wazazi na walezi wao ili kuweza kupata uhalisia wa sasa.

“Wanafunzi watakutana na dodoso katika akaunti zao katika mtandao wetu wa maombi ya mikopo (OLAMS) na watapaswa kujaza. Wale ambao hawatajaza dodoso hili kwa njia ya mtandao tutasitisha mikopo yao na wale ambao baada ya uchambuzi tutabaini hawana uhitaji, nao tutasitisha mikopo yao na watapaswa kuanza kurejesha fedha walizokopokea,’ alifafanua.

HESLB ilianzishwa mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai mwaka 2005 kwa lengo la kutoa mikopo kwa watanzania wahitaji waliopata nafasi za masomo katika vyuo vya elimu ya juu na kukusanya mikopo iliyoiva kutoka kwa wadaiwa walionufaika na mikopo tangu mwaka 1994.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatatu ya Octoba 31


Saturday, 29 October 2016

Jaji Lubuva Ataka Tume ya Uchaguzi Ifumuliwe.......Apendekeza Wakurugenzi wa Halmashauri Wawekwe Kando Kwenye Usimamizi

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva ameitaka serikali kubadili muundo wa tume hiyo ili iwe na ofisi na watumishi katika kila halmashauri nchini na ofisi ya Zanzibar.

Amesema hatua hiyo itawezesha NEC kufanya kazi zake kwa uhuru zaidi, badala ya kutegemea wakurugenzi wa halmashauri (Ma-DED).

Alisema hayo jana mjini Dodoma wakati akikabidhi taarifa ya tathimini baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama.

Tathimini hiyo imetolewa ikiwa ni mwaka mmoja tangu Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli kutangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi huo. 
Lubuva alisema serikali ifanyie mapitio ya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 na Sheria ya Serikali za Mitaa Sura 292 ili kurekebisha vifungu vinavyokinzana.

“Pamoja na hayo, serikali inatakiwa kubadili muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kuwa na ofisi na watumishi katika kila halmashauri nchini na ofisi ya Zanzibar, hiyo itafanya tume ifanye kazi zake kwa uhuru zaidi tofauti na sasa kazi hizo zimekuwa zikifanywa na wakurugenzi wa halmashauri,” alisema.

Alisema baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, tume iliamua kufanya tathimini kwa lengo la kupata mrejesho juu ya utekelezaji wa Uchaguzi Mkuu kutoka kwa wadau. Alisema ni mara ya kwanza kwa tume kufanya tathimini tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993.

“Tathimini hii imefanyika ikiwa ni mojawapo ya zoezi linalokamilisha mzunguko wa uchaguzi na kuanza kwa mchakato wa uchaguzi mwingine,” alisema.

Alisema changamoto zilizojitokeza kwa mujibu wa wadau waliohojiwa ni pamoja na mpiga kura kutoruhusiwa kupiga kura katika eneo tofauti na lile alilojiandikisha.

Pia wapiga kura kushindwa kupiga kura siku ya uchaguzi kutokana na kugawa mipaka ya kiutawala na majimbo ya uchaguzi, baada ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura na muda mfupi uliotolewa kujiandikisha na uwekaji wazi wa daftari la awali la wapiga kura.

Alisema tathimini inaonesha katika baadhi ya maeneo, watu waliojitokeza kupiga kura ni wachache, ukilinganisha na idadi ya wapiga kura waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

“Baadhi ya sababu zilizotolewa ni pamoja na uelewa mdogo juu ya umuhimu wa kupiga kura kutokana na elimu ya mpigakura kutowafikia wapigakura wengi, pia wapigakura walijiandikisha katika daftari la kudumu kwa ajili ya matumizi mengine ili kupata kadi kwa ajili ya matumizi mengine na uwepo wa hofu, vitisho na vurugu siku ya kupigakura,” alisema.

Waziri Mhagama, Mkurugenzi wanena
Kwa upande wake, Waziri Mhagama alisema tume inapaswa kupongezwa kwa kukamilisha zoezi zima la Uchaguzi Mkuu, ambalo lilikuwa na changamoto nyingi na ushindani mkubwa wa kisiasa.

Alisema kwa mujibu wa Kifungu cha 15(5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura 343, tume inapaswa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura mara mbili kati ya Uchaguzi Mkuu mmoja na mwingine, lakini haikuwezekana kufanyika hivyo baina ya mwaka 2010 na mwaka 2015 kutokana na sababu mbalimbali.

Alisema sababu hizo ni pamoja na ufinyu wa bajeti na kuchelewa kupatikana kwa fedha kwa wakati, lakini serikali itajitahidi kuhakikisha kuwa mapungufu yaliyo ndani ya uwezo wake, yanatatuliwa ili kuiwezesha tume kutekeleza majukumu yake ya kikatiba na kisheria kwa wakati.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima alisema tathimini ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ilifanyika, ikiwa ni hatua ya kukamilisha mzunguko wa uchaguzi.

Alisema kati ya watendaji 1,029 waliohojiwa, watendaji 929 ambao ni sawa na asilimia 90.3 walisema wana uelewa kuhusu muundo wa tume na watendaji 100 sawa na asilimia 9.7, walikuwa hawana uelewa kuhusu muundo wa tume.

“Kati ya watendaji 929 wa uchaguzi waliohojiwa, 818 sawa na asilimia 88 walisema kuwa muundo wa tume unafaa kuendesha uchaguzi, aidha watendaji 111 sawa na asilimia 12 walieleza kuwa muundo wa tume haufai katika kuendesha uchaguzi,” alisema.

Pia matokeo yanaonesha kuwa, katika watendaji wa uchaguzi 1,014 waliohojiwa, 814 sawa na asilimia 80.3 walisema hakukuwa na changamoto katika njia hizo, watendaji 200 sawa na asilimia 19.7 walieleza njia za mawasiliano zilikuwa na changamoto.

Alisema matokeo ya tathimini yameonesha kati ya watendaji 1,029 waliohojiwa 996 sawa na asilimia 96.8 walikuwa na maoni kuwa utekelezaji wa majukumu ya uchaguzi ulizingatia maelekezo yaliyotolewa na tume, ambapo watendaji 33 sawa na asilimia 3.2 walieleza kuwa utekelezaji haukuzingatia maelekezo hayo.

Aidha alisema wadau wa uchaguzi 1,915 waliohojiwa kuhusu uelewa wao juu ya elimu ya mpiga kura, kati ya wadau 1,463 sawa na asilimia 76.4 walisema walikuwa na uelewa wa elimu ya mpiga kura na 452 sawa na asilimia 23.6 hawakuwa na uelewa.

Kailima alisema wapiga kura 499 walihojiwa, ambapo kati yao wapiga kura 377 sawa na asilimia 75.6 walisema walitumia chini ya dakika 30 kufika kituo cha kupiga kura, wakati wapiga kura 87 sawa na asilimia 17.5 walitumia dakika 30 hadi 60 kufika kituo cha kupiga kura.

Taarifa ya Mamlaka ya Dawa na Chakula TFDA kuhusu Dawa bandia zilizokamatwa


Na Ally Daud-Maelezo
MADAWA bandia na yasiyo sahihi kwa matumizi ya binadamu yamekamatwa maeneo ya Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini baada ya kufanyika ukaguzi maalum wa kutafuta dawa bandia katika maeneo hayo iliyofanyika hivi karibuni.
 
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Bw. Hiiti Sillo wakati wa kutoa Matokeo ya ukaguzi maalum wa dawa uliofanyika katika mikoa ya Kanda za Ziwa na Nyanda za Juu Kusini.
 
“Kutokana na ukaguzi maalum tulioufanya katika Kanda za Ziwa pamoja na Nyanda za Juu Kusini wa kutafuta dawa bandia na zisizo sahihi kwa matumizi ya binadamu tumefanikiwa kukamata dawa bandia za aina tano ambazo zipo kwenye makundi mawili ya Dawa za malaria na Viua vijasumu(Antibiotics)” alisema Bw. Sillo.
 
Aidha Bw. Sillo amesema kuwa ukaguzi huo maalum umeweza kusaidia kukamata dawa ya malaria aina ya vidonge vya Quinine ambayo inadaiwa kutengenezwa katika kiwanda cha Elys Chemical  nchini Kenya na nyingine zinatengenezwa hapa nchini katika kiwanda cha Shelys Phamaceuticals Ltd.
 
Mbali na hayo Bw. Sillo amesema kuwa pamoja na kukamata dawa bandia pia zoezi hilo lilifanikiwa kubaini na kukamata dawa zilizoisha muda wa matumizi , zisizosajiliwa na zenye ubora duni zenye thamani ya Tsh. Milioni 17.463.
 
Bw. Sillo ameongeza kuwa Ukaguzi huo ulitokana na kuwa na taarifa za awali ambazo zilionyesha uwepo wa dawa bandia katika maeneo ya Geita na Mara mwezi Agosti na Septemba mwaka huu  na kusistiza kwamba zoezi hilo la ukaguzi linaendelea nchini kote na watakaokutwa na hatia watachukuliwa hatua stahiki.
 
Kwa upande wa Msajili wa  Baraza la famasi Bi. Elizabeth Shekalaghe amesema kuwa wataalamu wa madawa watakaokutwa na hatia ya kusambaza na kuhudumia dawa bandia watafutiwa usajili na kuacha kutoa huduma  kwa mujibu wa sheria ya dawa , chakula na vipodozi.
 
“Wataalamu wa dawa ambao wanasambaza na kuhudumia dawa bandia watafutiwa usajili na kuacha kutoa huduma  kwa mujibu wa sheria ya dawa , chakula na vipodozi pindi watapogundulika” alisema Bi. Shekalaghe.
 
Zoezi hilo la Ukaguzi maalum wa dawa bandia ulianza Oktoba 4 mwaka huu linafanywa kwa ushirikiano wa TFDA, Jeshi la polisi pamoja na Maafisa kutoka Baraza la Famasi litakuwa endelevu ili kuhakikisha dawa bandia zinatoweka nchini.

Mmiliki wa Shule Iliyofutiwa Matokeo Ya Darasa la 7 Amwaga Machozi Hadharani

Siku moja baada ya matokeo ya darasa la saba kutangazwa, baadhi ya wamiliki wa shule wamelijia juu Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kwa kufuta matokeo ya wanafunzi wao, huku mmoja wao akibubujikwa na machozi akidai wamehujumiwa.

Ikitangaza matokeo hayo juzi, Necta ilisema imefuta matokeo ya wanafunzi 238 kwa sababu ya udanganyifu, ikiwatuhumu wakuu wa shule sita na walimu kuhusika kuiba mitihani, kuwapa majibu watahiniwa au kuwafanyia mtihani.

Necta ilienda mbali zaidi na kudai kuwa kwenye shule moja, walimu walijificha bwenini, chooni na ofisini ambako wanafunzi waliwafuata na kupewa majibu na baadaye kuyasambaza kwa wenzao.

Lakini, walimu hao  wamepinga vikali tuhuma hizo za kushiriki katika udanganyifu, isipokuwa shule moja tu ambayo ilisema mwalimu aliyehusika ameshachukuliwa hatua.

“Sijafurahishwa na kitendo cha Necta kuifutia matokeo shule yetu. Hiyo ni hujumu,” alisema mmiliki wa shule ya msingi Tumaini iliyopo Sengerema mkoani Mwanza, Kandumula Maunde.

Huku akilia, Maunde alisema wakati tukio hilo lilotokea saa 5:00 asubuhi, hakuwepo na hakushirikishwa.

“Niliitwa kesho yake na kupata maelezo kuwa wanafunzi wa shule yako wamekamatwa kwa sababu wameandikiwa majibu ya mtihani kwenye sketi, sikukubaliana nao,” alisema.

Kwa mujibu wa Necta, mmiliki huyo aliiba na kuandaa majibu ambayo watahiniwa wake waliandika kwenye sare za shule na kuyatumia ndani ya chumba cha mtihani.

Necta imewataja waliohusika kuwa ni mmiliki aliyetajwa kwa jina la Jafari Maunde, msimamizi anayeitwa Alex Kasiano Singoye na wanafunzi wote.

Alisema hakukubaliana na kitendo hicho kwa sababu wanafunzi hao walikuwa wameandaliwa vizuri kujibu mitihani yao.

Maunde aliliomba baraza la mitihani kupitia upya uamuzi wake wa kuifutia shule hiyo matokeo kwa kuwa umeathiri maisha ya wanafunzi waliokuwa na ndoto za kuendelea na masomo.

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo waliofutiwa matokeo waliiomba Necta kuangalia upya uamuzi huo. Wanafunzi hao walieleza kuwa msimamizi wa mtihani wa siku hiyo alikuwa akiwasumbua na aliwalazimisha waandike maelezo ya kukiri kuwa walikamatwa na majibu.

“Msimamizi alitulazimisha tuandike kwenye ubao baada ya kumaliza mitihani maelezo yakisema tumekamatwa na majibu ya mtihani yakiwa yameandikwa kwenye sketi tulizokuwa tumevaa,” alisema mmoja wa wanafunzi hao, Kefa Matini.

Kwa upande wa shule ya msingi ya Little Flower iliyopo Serengeti mkoani Mara, walimu walisema uamuzi wa kufutiwa matokeo ni adhabu isiyostahili.

Wanafunzi 37 wa shule hiyo  inayomilikiwa na Kanisa Katoliki, Parokia ya Magumu wamefutiwa matokeo. 

Necta imeeleza kuwa mwalimu mkuu wa Little Flowers aliiba mtihani, kuandaa majibu na kumpa msimamizi mkuu pamoja na wasimamizi wengine ili wawape watahiniwa.

Imesema waliohusika ni mwalimu mkuu anayeitwa Cecilia Nyamoronga, msimamizi mkuu (mwalimu), Haruni Mumwi na msimamizi (mwalimu), Genipha Simon na watahiniwa wote.

Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo, Paskael Chacha alisema uamuzi huo umewaumiza walimu na watoto waliofanya mtihani walioko shuleni na wazazi kwa kuwa hawajapewa sababu za udanganyifu huo na ulimhusisha nani na lini.

“Walimu hawakuwepo shuleni, mkuu wa shule ndiye alikuwa akiruhusiwa kuwepo shuleni kwa muda mfupi. Inanipa shida kujua udanganyifu ulifanyikaje na ulimhusisha nani.

"Hili suala linatupa shida kwa kuwa wasimamizi walioletwa siku ya kwanza si waliofika kusimamia. Sasa taarifa kama hizi zinauma sana,” alisema.

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa taarifa zinazodai kuwa siku ya mtihani mtoto mmoja alikamatwa na karatasi ya majibu na kumtaja mkuu wa shule kuwa ndiye aliyempa, mwalimu huyo alikana na kudai kuwa hana taarifa.

Majibu ya Dr. Msonde
Akizungumzia malalamiko hayo, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema wanaosema wameonewa wanatakiwa kuomba radhi na kukubali adhabu kwa sababu waliokamatwa walikutwa na uthibitisho, akitoa mfano wa Shule ya Msingi Tumaini.

Kwa upande wa Shule ya Msingi Little Flower, Dk Msonde alisema ofisa wa baraza la mitihani alishuhudia mwalimu akipitisha karatasi ya majibu kwa wanafunzi .

“Sasa hapo utasema umeonewa? “Tumezoea kuona (matukio ya udanganyifu) yale ya mwanafunzi mmoja, lakini haya yanatisha. Mwalimu au msimamizi anamsaidia mwanafunzi, hii si sawa,” alisema.

Serikali Yarejesha asilimia 52 ya hisa zake UDA


Serikali imefanikiwa kurejesha udhibiti wake kwenye Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) baada ya kurejeshewa asilimia 52 ya hisa zilizonunuliwa kinyume na utaratibu na Kampuni ya Simon Group Limited (SGL). 
 
Kurejeshwa kwa hisa hizo kunatokana na ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwamba mauzo ya hisa hizo yaliyofanywa na Bodi ya Wakurugenzi wa Uda hayakuwa na kibali cha Serikali. 
 
Ripoti ya CAG ya mwaka 2014/15 ilibainisha licha ya utaratibu kukiukwa pia hakuna vilelezo vya fedha za manunuzi zaidi ya kuonyesha Sh320 milioni ziliingizwa kwenye akaunti binafsi ya Mwenyekiti wa Bodi, Idd Simba ambazo hata hivyo alidai ni malipo ya ushauri alioutoa kwa mwekezaji huo. 
 
Kurejeshwa kwa hisa hizo, kutolewa taarifa ndani ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambayo Jumanne ya wiki hii iliuweka kikaangoni uongozi wa Jiji la Dar es Salaam kuhusiana na sakata la Uda. 
 
Pia, kamati iliwataka Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) George Simbachawene, Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju na Msajili wa Hazina Lawrence Mafuru wafike kwenye kamati wakiwa na majibu sahihi kuhusu sakata hilo.
 
 Viongozi hao waliitikia wito huo jana, na baada ya kikao cha faragha Mwenyekiti wa LAAC , Vedasto Mwiru alisema Serikali imeitaarifu kamati yake kuwa imerejesha katika himaya yake fungu kuu la hisa ambazo hazikugawiwa. 
 
Mwiru alisema Serikali imerejesha hisa asilimia 52 ambazo ziliuzwa na Bodi ya Wakurugenzi Wa Uda kinyume cha utaratibu. 
 
“Maelezo yaliyotolewa na Serikali zile share (hisa) zote  ambazo hazikugawiwa ziko salama chini ya mikono  salama ya Serikali hazijauzwa,” alisema. 
 
Mwiru ambaye pia ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CUF), alisema kutokana na maelezo hayo wabunge wametaka mikataba ya kurudisha hisa hizo kwa Serikali ipelekwe kwenye kamati hiyo. 
 
Alisema kamati hiyo inaipa Serikali muda wa wiki mbili kuhakikisha kuwa wanawasilisha nyaraka hizo. 
 
Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita alisema wanasubiri majibu ya barua yao ya kuomba ushauri kuhusu uuzwaji wa hisa za jiji za asilimia 51 kutoka kwa mwanasheria Mkuu wa Serikali.
 
Alisema baada ya kupokea ushauri huo watapeleka katika Baraza la Madiwani ili kuona namna ya kwenda mbele pamoja na kuzifanyia kazi fedha walizouza hisa zao ambazo ziko katika Benki Kuu (BoT). 
 
Mwanasheria Mkuu Masaju alisema anakwenda kuandika mambo yote yaliyosemwa ili iwasaidie kamati na Jiji la Dar es Salaam kukamilisha utaratibu huo kisheria.

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumamosi ya Octoba 29