Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Elimu, Joseph Mungai unatarajiwa kuagwa Dar es Salaam leo katika viwanja vya Karimjee.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, mtoto wa marehemu, William Mungai alisema
ibada ya kuuaga mwili huo itafanyika katika viwanja hivyo saa 5.00
asubuhi.
Hata
hivyo mtoto huyo wa marehemu hakutaka kuingia kwa undani kuhusu chanzo
cha kifo cha baba yake, badala yake alisema familia iachwe iendelee
kushauriana na daktari.
Alisema
pamoja na hayo, kifo hicho kimewashtua kwa vile kimetokea ghafla na
kwamba baada ya kuisha kwa ibada ya kuaga mwili huo, utasafirishwa hadi
Mafinga, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa kwa mazishi.
“Hadi
sasa familia tunajua kwamba marehemu aliugua tumbo la kawaida na
tulimpeleka hospitalini ambako alifariki dunia, tunaomba familia iachwe,
kwa sababu bado tunashauriana na daktari wake.
“Tumekubaliana mwili wake uagwe kesho (leo) saa tano Viwanja vya Karimjee ambako pia historia yake yote na familia itasomwa,” alisema William.
Kifo
cha Mungai kilitokea juzi jioni katika kile kilichoelezwa kuwa
alianza kujisikia vibaya baada ya kunywa kiywaji katika hoteli moja
iliyopo Msasani, ambayo aliizoea.
Mmoja
wa waombelezaji waliofika nyumbani kwa marehemu jana ni pamoja na Naibu
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)- Zanzibar,
Salum Mwalimu ambaye alimwelezea Mungai kuwa aliunga mkono mabadiliko
ya siasa.
“Hakuwa
na kadi ya Chadema lakini alipenda mabadiliko, mwanaye William
aligombea ubunge wa Mafinga kupitia Chadema na baba yake alimuunga
mkono,” alisema.
Mbunge
wa zamani wa Kwela, Chrisant Mzindakaya alisema amesikitishwa na kifo
hicho ikizingatiwa wiki iliyopita walikuwa pamoja na walizungumza mambo
mengi ya siasa.
“Hakuwa
na kesho katika maisha yake, alilokuwa na uwezo wa kulifanya alilifanya
siku hiyo hiyo, alikuwa na msimamo, hakukubali kuyumbishwa,” alisema Mzindakaya.
Wakati
huohuo, mwili wa aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta unatarajiwa
kuwasili leo ukitokea Ujerumani ambako alikuwa akitibiwa hadi mauti
yalipomfika.
Taarifa
zilizotolewa na msemaji wa familia ya marehemu, Gerald Mongella,
zinasema mwili huo utawasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere saa 9.00 mchana na kupelekwa nyumbani kwake Msasani, Dar
es Salaam.
“Ijumaa(kesho)
saa tatu asubuhi ibada ya kuuaga mwili huo itafanyika katika viwanja
vya Karimjee ambako ndugu na wakazi wa Dar es Salaam watapata fursa ya
kuaga,” alisema Mongella.
Mwili
wa Sitta utasafirishwa hadi Dodoma ambako utaagwa na wabunge na baadaye
utasafirishwa kwenda Urambo kwa mazishi Jumamosi.
Sitta
alifariki Novemba 07 mwaka huu katika Hospitali ya Technal University
alipokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya saratani ya tezi dume.
No comments:
Post a Comment