MBUNGE
wa Bunda Mjini, Ester Bulaya (Chadema), ameiambia Mahakama Kuu Kanda
ya Mwanza, kwamba alishinda uchaguzi wa ubunge uliofanyika mwaka jana.
Bulaya
aliyasema hayo mahakamani hapo jana mjini Musoma kupitia kwa wakili
wake, Tundu Lissu, mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga,
Noel Chocha, anayesikiliza kesi ya kupinga matokeo yake iliyofunguliwa
na aliyekuwa mgombea wa CCM, Stephen Wassira.
Katika
utetezi wake baada ya kuapa, Bulaya alisema alitangazwa na msimamizi wa
uchaguzi wa jimbo hilo baada ya taratibu zote ikiwamo kuhesabu kura,
kukamilika.
Baada
ya utetezi huo, malumbano ya sheria baina ya mawakili wa upande wa
waleta maombi na wajibu maombi yaliibuka na kudumu kwa zaidi ya saa
tatu.
Malumbano
hayo yalianza baada ya Wakili wa Waleta maombi, Costantine Mutalemwa,
kuiomba mahakama hiyo iondoe aya saba kati ya 11 zilizokuwa kwenye
utetezi wa Bulaya kwa kile alichodai hazimo kwenye utaratibu wa awali
uliowasilishwa mahakamani hapo.
Aya
ya saba ya utetezi wa Bulaya inadai kasoro ya kura 164,794
zilizotangazwa awali na msimamizi wa uchaguzi badala ya kura 69,369 za
wapiga kura halali, hazikuathiri matokeo.
Wakili
Mutalemwa alidai kwamba, madai yaliyotokea kwenye utetezi wa mbunge
huyo ni mapya na suala la idadi ya wapiga kura ni moja ya kipengele
ambacho wateja wake wanakipinga.
“Naomba
mheshimiwa jaji aya ya pili, tatu, nne, tano, sita, saba na nane,
ziondolewe kwenye utetezi wa Bulaya na zibaki aya ya kwanza, ya tisa, ya
10 na aya ya 11.
“Naomba aya hizo ziondolewe kwa sababu ni mpya na hazipo kwenye utaratibu wa awali,” alidai Wakili Mutalemwa.
Kutokana na maombi hayo, Lissu alisema hakubaliani na pingamizi la wakili huyo.
Alisema
amekumbuka kauli ya aliyekuwa Rais wa iliyokuwa Mahakama ya Afrika
Mashariki, Sir Charz Nyubon aliyewataka mawakili wasiweke mapingamizi
yasiyo na msingi.
“Kitendo
cha mawakili kuweka mapingamizi yasiyo na msingi ni kupoteza muda wa
mahakama kwa mujibu wa kauli ya rais huyo na nakuomba mheshimiwa jaji
uendelee na ushahidi wa mtoa ushahidi kwa kuwa muda wa kupoteza kwenye
ushahidi haupo,” alisema Lissu.
Naye
Wakili wa Serikali, Angela Lushagamba, alisema hana pingamizi lolote
kwenye kiapo cha utetezi wa Bulaya uliotolewa mahakamani hapo na kuiomba
mahakama iendelee kusikiliza ushahidi.
Akitoa
uamuzi juu ya hoja zilizoibuka mahakamani hapo, Jaji Chocha, alisema
anaona dalili za shauri hilo kusikilizwa kwa muda mrefu kutokana na hoja
mpya zilizoibuka mahakamani.
“Kuna vitu vipya ambavyo vimeibuka kwa siku ya leo na nahitaji nipate muda zaidi ya saa tano kuvifanyia kazi,” alisema Jaji Chocha huku akiahirisha kesi hiyo hadi leo saa saba mchana.
No comments:
Post a Comment