Watanzania
wanakumbuka kuwa mnamo tarehe 10 Septemba, 2016 lilitokea tetemeko la
ardhi katika eneo la Kanda ya Ziwa na hususan Mkoa wa Kagera.
Tetemeko
hilo lilisababisha athari mbalimbali zikiwemo vifo, majeruhi, uharibifu
wa makazi na miundombinu ya umma na watu binafsi. Jumla ya Watu 117,721
wameathirika kwa kupoteza makazi yao, mali na athari za kisaikolojia
katika Wilaya za Bukoba, Missenyi, Muleba, Karagwe na Kyerwa.
Aidha,
jumla ya watu 17 walipoteza maisha na 560 walijeruhiwa. Vilevile,
nyumba 2,072 za makazi zilianguka kabisa na nyumba 14,595 za makazi
zilibomoka, baadhi zina kuta au kupata nyufa kubwa na hivyo kuzifanya
kuwa hatarishi kwa makazi ya binadamu. Vilevile, maafa haya
yalisababisha uharibifu mbalimbali wa miundombinu ya barabara na majengo
ya watu na taasisi mbalimbali, ikiwemo shule na Hospitali.
Kufuatia
maafa hayo, wananchi na taasisi mbalimbali, pamoja na nchi marafiki,
waliitikia wito wa kuwasaidia wahanga wa maafa na kukarabati miundo
mbinu iliyoharibika. Hadi kufikia mwezi Oktoba, Fedha, Vyakula na Vifaa
mbalimbali vya Ujenzi vilikuwa vimepatikana kwa njia ya michango
mbalimbali.
Chama
chetu kimeshtushwa na kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera kwamba Wananchi
walioathirika wajitegemee wenyewe na kwamba misaada yote iliyotolewa Ni
ya Serikali na Taasisi zake tu. Kauli hii ya Mkuu wa Mkoa haikubaliki
kwani inadhalilisha waathirika na watu wote waliojitoa kuwasaidia
waathirika hao.
Tunachukulia
kauli hii kama tangazo la wizi wa uaminifu wa wananchi waliochanga. Ni
busara ya kawaida kuwa hatua ya kwanza katika kushughulikia maafa ni
kurudisha hali ya maisha ya watu katika hali ya kawaida sambamba na
ukarabati wa miundombinu. Aidha, suala la ujenzi wa miundo mbinu ya
taasisi za umma ni jukumu la msingi la serikali. Kwa sababu hii:
•
ACT Wazalendo tunaitaka serikali kuu kujitenga na kufuta kauli ya mkuu
wa mkoa wa Kagera kwa sababu inaigombanisha serikali na wananchi
inaowaongoza.
•
ACT Wazalendo tunaitaka serikali kuelekeza ni misaada iliyopatikana kwa
michango ya wananchi, taasisi na nchi rafiki katika kusaidia wananchi
walioathirika kurudi katika maisha ya kawaida, ikiwemo ukarabati na
ujenzi wa nyumba za kuishi.
•
ACT Wazalendo tunatoa wito kwa taasisi za kiraia nchini kuchukua nafasi
yake katika kuendelea kuikumbusha serikali wajibu wake wa msingi wa
kuboresha maisha ya watu.
Janeth Rithe
Katibu wa Taifa ACT Wazalendo, Kamati ya Maendeleo ya Jamii
13/11/2016, Dar Es salaam.
No comments:
Post a Comment