Wakati
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema (40) akitarajia kujua
hatima ya dhamana yake katika Mahakama Kuu leo, kesho yeye na mkewe
Neema Lema (33) watapanda kizimbani kwa kesi ya uchochezi dhidi ya Mkuu
wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.
Ijumaa
iliyopita Lema alipelekwa Gereza la Kisongo, Arusha baada ya kunyimwa
dhamana katika kesi nyingine ya kutoa kauli za uchochezi dhidi ya Rais
John Magufuli, hatua ambayo imepingwa na chama chake na mawakili wake.
Katibu
wa Chadema Mkoa wa Arusha, Calist Lazaro alisema hawakuridhishwa na
pingamizi la dhamana lililowekwa na mawakili wa Serikali kwani tayari
Lema alikuwa amepewa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi.
“Tayari tumefanya mazungumzo kuongeza nguvu za mawakili wa chama ambao wataungana na mawakili wa Arusha kudai dhamana leo,” alisema.
Mmoja
wa mawakili hao, Shaki Mfinanga alisema leo wanatarajia kuwasilisha
maombi ya dhamana ya Lema wakiwa na mawakili wa Chadema.
Kesi ya mkewe
Wakati
hayo yakiendelea, kesho Lema na mkewe watakuwa mahakamani mbele ya
kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa Arusha, Desdery Kamugisha.
Katika
kesi hiyo, Hakimu Kamugisha amewapa dhamana washtakiwa hao katika kesi
ya kusambaza ujumbe kumkashifu mkuu wa Mkoa Arusha.
Lema
anadaiwa kuwa Agosti 20, 2016 akitumia simu namba 076415**47 ambayo
imesajiliwa kwa jina la mkewe, alituma ujumbe kwenye namba ya Gambo 0766
75**75 wenye maneno ya uchochezi.
Maneno hayo; “Karibu Tutakudhibiti kama Uarabuni walivyodhibiti Mashoga”
yanadaiwa ya uchochezi kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni za Adhabu,
Kifungu cha 118 (a) na Kifungu cha tatu katika sheria iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2010.
Katika
shtaka jingine, Lema anashtakiwa peke yake, akituhumiwa kivunja Sheria
ya Makosa ya Jinai namba 390 kifungu cha 35 kwa kuhamasisha maandamano
kinyume cha sheria wakati wa mkakati ulioitwa Ukuta na chama hicho.
Lema
alidaiwa kutenda kosa hilo kati ya Agosti Mosi hadi 26 kwa kusambaza
ujumbe kupitia mtandao wa WhatsApp wakati akijua kufanya ni kosa
kisheria. Katika kesi hiyo, Lema na mkewe wanatetewa mawakili wanne,
John Mallya, James Lyatuu, Reygod Nkya na Mfinanga.
No comments:
Post a Comment