Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia
salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Job Ndugai kufuatia kifo cha Spika Mstaafu na Mbunge Mstaafu wa
Jimbo la Urambo lililopo Mkoani Tabora Mhe. Samwel Sitta.
Mhe.
Samwel Sitta amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya
Technical University of Munich nchini Ujerumani alikokuwa akipatiwa
matibabu tangu mwezi uliopita.
Katika
salamu hizo, Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshtuko na masikitiko
makubwa taarifa za kifo cha Mhe. Samwel Sitta na kwamba Taifa
limempoteza mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa katika uongozi na
maendeleo.
“Nitamkumbuka
Mzee Sitta kwa uchapakazi wake, uzalendo wake na tabia yake ya
kusimamia ukweli katika kipindi chote alichokuwa kiongozi katika ngazi
mbalimbali za siasa na Serikali.
“Kupitia
kwako Mhe. Spika naomba kutoa pole nyingi kwa Mke wa Marehemu Mhe.
Magreth Sitta ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Urambo na familia nzima ya
marehemu, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wananchi
wa Urambo Mkoani Tabora na watu wote walioguswa na msiba huu” amesema Rais Magufuli katika salamu hizo.
Dkt.
Magufuli amesema anaungana na wafiwa wote katika kipindi hiki kigumu
cha maombolezo na amewaombea moyo wa uvumilivu na ustahimilivu.
“Namuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Marehemu mahali pema peponi, Ameni”
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
07 Novemba, 2016
No comments:
Post a Comment