Serikali
imeitaka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na wadau wa
maendeleo nchini ikiwemo Shirika la Maendeleo ya Viwanda Duniani (UNIDO)
na Shirikisho la Viwanda Nchini (CTI) kuendelea kufanya utafiti ili
kubaini idadi na maendeleo ya viwanda vidogo vilivyopo nchini.
Hayo
yamesemwa jana Jijini na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt
Charles Mwijage wakati wa uzinduzi wa matokeo ya Sensa ya Uzalishaji
bidhaa Viwandani mwaka 2013.
Dkt
Mwijage alisema kuwa katika mataifa yanayoendelea duniani ikiwemo Korea
Kusini, Malaysia na Singapore uchumi wa nchi hizo umeweza kukua kwa
kiwango kwa juu zaidi kutokana na kuweka mkazo katika kuendeleza viwanda
vidogo na vya kati.
Alisema
katika kuharakisha kasi ya maendeleo ya viwanda vidogo nchini, Wizara
yake imekusudia kuwajengea hamasa Watanzania kupendelea kujenga viwanda
vidogo vidogo na vya kati, kwani kukua kwa sekta ya viwanda nchini
kutaisaidia kuinua uchumi wanchi.
“Asilimia
25- 40 ya mazao ya kilimo yanayovunwa huharibika kabla ya kufikishwa
kiwandani, katika kukabiliana na hali hiyo Serikali imekusudia kujenga
viwanda vidogo vidogo ili kuwawezesha wakulima wapate sehemu nzuri zaidi
za kuhifadhi mazao yao” alisema Mwijage.
Aidha,
Dkt Mwijage alisema, sekta ya viwanda vidogo vidogo nchini imeendelea
kukua kwa kasi nchini ambapo hadi sasa kuna jumla ya viwanda 3800
vilivyoanzishwa nchini kuanzia Novemba 2015 hadi oktoba, 2016.
Katika
hatua hiyo Dkt Mwijage alisema kuwa Wizara yake inaendelea kuhamasisha
Sekta binafsi kuwekeza katika Sekta ya viwanda vidogo, vya kati na
vikubwa ikiwa jukumu kuu la Serikali ni kuhakikisha nchi inakuwa salama
na inajenga mazingira wezeshi kwenye sekta binafsi kuzalisha na kufanya
biashara.
Naye
Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa
alisema kuwa matokeo hayo yanaonyesha mafanikio katika sekta ya viwanda
ikiwemo kuongezeka kwa ajira zipatazo 264,223 nchini na kuchangia uchumi
kwa takribani Shilingi bilioni 8.0 kwa mwaka 2013.
Alisema
kuwa Takwimu za matokeo ya sensa ya uzalishaji viwandani ni rasmi na
kuwataka watunga sera, wanasiasa, viongozi, sekta binafsi na watu
binafsi kutumia matokeo hayo kwa lengo la kuboresha Sekta ya viwanda
nchini.
Na Beatrice Lyimo, MAELEZO
No comments:
Post a Comment