Na Jacquiline Mrisho na Eleuteri Mangi – MAELEZO, Dodoma.
Mkutano
wa Tano wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umepitisha
rasmi Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 ambapo hatua
inayofuata ni kuridhiwa na kusainiwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli
ili uwe Sheria kamili ya nchi.
Muswada huo umepitishwa jana Bungeni mjini Dodoma ambapo mkutano huo uliongozwa na Mwenyekiti wa Bunge hilo, Mhe. Andrew Chenge.
Wabunge
walijadili Muswada huo kifungu kwa kifungu na kuunga mkono upitishwaji
wake baada ya Waziri mwenye dhamana na habari kutoa hoja ili Muswada huo
uweze kujadiliwa.
Akiongea
na waandishi wa habari mara baada ya kupitishwa Muswada huo, Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye aliwashukuru wadau
wote walioshiriki katika kutoa maoni juu ya Muswada huo kwani ndiyo
yamepelekea kukamilisha mchakato mzima wa Muswada huo.
“Kwa
niaba ya Serikali napenda kuwashukuru wadau wote walioshiriki kwa namna
moja au nyingine katika kuhakikisha tunatimiza malengo ya takribani
miaka 20 iliyopita ya kuifanya taaluma hii ya habari kuheshimika kama
zilivyo taaluma zingine”, alisema Waziri Nape.
Waziri
Nape aliongeza kuwa kwa sasa Muswada huo umeshapitishwa hivyo
kilichobaki ni utungaji wa Kanuni ambapo ameomba wadau wa tasnia ya
habari kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kutoa maoni yatakayopelekea
kuwa na kanuni zenye tija kwa wanahabari na taifa kwa ujumla.
Aidha,
Mhe. Nape aliwaasa wadau wa habari kuunganisha nguvu kwa pamoja hasa
katika kipindi hiki ambacho Muswada huo umepitishwa pia amewataka wadau
hao wasiruhusu mgawanyiko utokee kati yao bali washirikiane na Serikali
katika kutekeleza wajibu wao wa kihabari kwa jamii.
Kwa
upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju alisema kuwa
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 ni mwanzo mpya wa
tasnia ya habari nchini ambapo aliwaasa wadau wa habari wakiwemo
waandishi wa habari kutambua kuwa haki mara zote huendana na wajibu,
hivyo hakuna haki isiyo na wajibu.
Muswada
huo uliopitishwa jana umejadiliwa na Bunge hilo kwa siku mbili ambapo
kwa mara ya pili ulisomwa mbele ya Kamati ya Bunge zima na hatimaye
kusomwa kwa mara ya tatu ili kukidhi hatua za utungwaji wa Sheria
nchini.
No comments:
Post a Comment