Mbunge
wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ameamua kufunga ili kuwa
karibu na Mungu wakati akiendelea kushikiliwa na polisi mkoani Arusha.
Wakati
Lema akiamua kufanya hivyo, taarifa zilizopatikana mjini Arusha
zinaeleza kuwa polisi walikwenda naye nyumbani kwake kwa ajili ya
upekuzi lakini hawakufanikiwa kupata chochote.
Kamanda
wa polisi wa Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo hakuweza kupatikana
kuzungumzia suala hilo na hata alipotafutwa kwa simu, hakupokea.
Suala
la Lema kuacha kula ili awe karibu zaidi na Mungu lilielezwa na
mwenyekiti wa Chadema wa mkoa, Amani Golugwa ambaye alisema ameelezwa na
mke wa mbunge huyo.
Lema,
ambaye alikamatwa Jumatano iliyopita mkoani Dodoma na kuletwa mjini
hapa Alhamisi, bado hajafikishwa mahakamani. Imeelezwa kuwa viongozi wa
chama chake wameshindwa kumuona kutokana na kuzuiwa na polisi.
Akizungumzia
suala hilo jana, Golugwa alisema alipokea ujumbe kutoka kwa mke wa
mbunge huyo, Neema Lema kuwa mumewe ameamua kufunga na kuomba kwa ajili
ya Taifa kuhusu mambo yanayoendelea na kuwa ameona kipindi hiki ambacho
yupo rumande ni cha kuwa karibu zaidi na Mungu.
“Kama
tunavyomjua Lema ni mtu anayempenda sana Mungu, ameamua kujinyenyekeza
mbele za Mungu. Anafunga na kuomba jioni mke wake anampelekea chakula na
amesema yupo katika hali nzuri,” alisema Golugwa.
Golugwa alisema wamejitahidi kutaka kumuona Lema, lakini wamegonga mwamba na wameshindwa kumwekea dhamana mbunge huyo.
Alisema
alizungumza na ofisa upelelezi wa makosa ya jinai mkoani hapa na
Kamanda Mkumbo, wote walisisitiza kuwa Lema ataendelea kuhojiwa hadi
watakapojiridhisha.
“Ni
jambo la kushangaza kama mtuhumiwa anaweza kukaa rumande zaidi ya saa
48 kama sheria inavyotaka, nadhani hapa siyo sheria tena, labda ni kwa
mujibu wa maelekezo ambayo hatujui yametoka wapi na kwa malengo yapi,” alisema Golugwa.
Alisema
baada ya kuwasili kutoka Dodoma alifanikiwa kuonana naye mara moja tu
na baadaye hakuna mtu aliyeruhusiwa kuonana naye; iwe viongozi wa
Chadema au wakili wa chama hicho, John Mallya ambaye ameshawasili kwa
ajili ya mambo ya kisheria .
Juzi,
Kamanda Mkumbo alisema Lema hataachiwa hadi upelelezi ukamilike na
mwanasheria wa Serikali atakapokuwa amemaliza kuandaa mashtaka kwa kuwa
amekuwa akirudia makosa yaleyale ya uchochezi.
No comments:
Post a Comment