Kwa
mamlaka iliyopewa kisheria kupitia kifungu namba 58(2) (a) na (b) cha
Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu inapenda
kuutarifu umma kwamba zoezi la tathmini ya hali ya kifedha ya Twiga
Bancorp Ltd (Twiga) limekamilika; kwa mantiki hiyo, Twiga itaanza kutoa
baadhi ya huduma za kibenki kwa umma kuanzia Jumanne tarehe 8 Novemba
2016.
Huduma
hizo ni pamoja na ukusanyaji wa marejesho ya mikopo ya wateja. Meneja
Msimamizi wa benki hiyo atawajulisha wateja huduma zitakazotolewa na
taratibu za kuzingatia.
Benki
Kuu ipo katika mchakato wa kupitia na kuchambua njia mbadala za kutatua
tatizo la mtaji linaloikabili Twiga Bancorp. Njia inayopewa kipaumbele
ni kutafuta mtaji kutoka kwa wawekezaji wapya, mchakato utakaowahitaji
kuchambua hali halisi ya taarifa za hesabu za Twiga (due diligence).
Zoezi
hili linatarajiwa kuchukua takribani wiki tatu na litakapokamilika,
Benki Kuu itaingia makubaliano na wawekezaji wapya kuhakikisha
wanaingiza mtaji unaohitajika haraka iwezekanavyo ili shughuli za
kawaida za kibenki ziweze kuendelea.
Benki
ya Twiga itaendelea kuwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu hadi hapo
utaratibu wa kuwamilikisha wawekezaji wapya utakapokamilika.
Benki
Kuu ya Tanzania ilitangaza kuiweka Twiga Bancorp Ltd chini ya usimamizi
wake kuanzia tarehe 28 Oktoba 2016 kutoka na upungufu mkubwa wa mtaji
unaoikabili.
Benki
Kuu ya Tanzania inapenda kuuhakikishia umma kuwa itaendelea kulinda
maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la kuleta ustahimilivu
katika sekta ya fedha.
BENKI KUU YA TANZANIA
6 Novemba, 2016
No comments:
Post a Comment